Akizungumza na wadau wa maendeleo katika ukumbi wa shule ya msingi Majimoto halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe Mkoa wa Katavi Mhe. Sanga amesema serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutoa huduma kwa jamii yake katika nyanja zote imiwemo afya, elimu, miundombinu ya barabara, umeme, maji na kutekeleza miradi mingine katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe.
Akifafanua umuhimu wa watoto kupatiwa nafasi ya kujiendeleza kielimu, Mhe Sanga amewataka wananchi hao kuwaandikisha wototo waliofikia umri wa kuanza darasa la awali huku wakizingatia umri sahihi wa watoto hao ili wapate msingi mzuri wa elimu kabla ya kuanza masomo ya darasa la kwanza kuliko kuwaacha nyumbani.
"Ninawaomba wazazi tuwe na mwamko wa elimu katika maeneo yenu, tuwapeleke watoto wetu wakapate elimu ya awali kabla ya kuanza masomo ya darasa la kwanza, kuliko kuwaacha majumbani mwetu wakitusaidia shughuli za familia hii haitatusaidia kuokoa kizazi hiki" Amesema Mhe. Sanga
Mhe. Sanga amewaomba wazazi wa wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka huu 2022 kuacha tabia ya kuwaachisha wanafunzi shule hasa kwa wale wanaotarajiwa kuanza masomo yao ya kidato cha kwanza januari 2023 kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwaozesha.
"Tutachukua hatua kali za kinidhamu kwa wazazi ambao kwa namna moja ama nyingine watakwamisha mwanafunzi kujiunga kidato cha kwanza 2023, ninazema haya kwa uchungu mkubwa nikiwa kama mzazi kwani kuna tabia za wazazi wasio na uchungu kwa watoto wao huwaozesha mapema ili kupata mali, ninalaani tabia na isitokee" Amesema Mhe. Sanga
"Matarajio ya rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona watoto wanaohitimu darasa la saba na kufaulu mtihani wao wote wanaingia kidato cha kwanza pasipo kupata kikwazo cha aina yoyote, na ndiyo maana serikali kuu kwa mwaka huu imetupatia kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 ili tuzisimamie kuhakikisha tunajenga vyumba vya madarasa ambayo watoto hawa watayatumia ifikapo 2023" Amesema Mhe. Sanga
Mhe. Sanga amewataka wananchi pia kujenga vyoo bora katika maeneo yao ili kuepuka magonjwa ya milipuko kama kipindupindu ambacho husababishwa na uchafu wa mazingira.
"Ndugu zangu wadau wa maendeleo ninawaomba tukaisaidie jamii kila mtu kwa nafasi yake kutoa elimu juu ya kuwa na vyoo bora na si bora choo katika makazi yetu, lakini kuepuka kushikana mikono ili kuepukana na magonjwa mbalimbali ikiwepo ugonjwa wa Ebora. Amesema Mhe. Sanga
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kuzingatia kanuni na taratibu za maswala ya lishe bora kwa jamii.
"Mpimbwe ni eneo ambalo linajitahidi kwa kulima mazao lakini wananchi hawazingatii kupata chakula bora, ulaji wa nyakula vilivyo poa au kula chakula kilicholala kikiwa cha baridi si afya bora kwa watoto wetu kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kwa watoto hao kupata matatizo ya utapia mlo, hivyo tujitahidi kurinda afya za watoto.
kwa upande wake mkurungenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe Bi. Catherine Mashalla amewasainisha mikataba watendaji wa vijiji na kata katika wilaya yake ili wakasimamie shughuli za masuala ya lishe mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Sanga.
Ikumbukwe kuwa Wilaya ya Mlele ina halmashauri mbili ambazo ni halmashauri ya wilaya ya Mlele na halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe, Mwaka 2021 halmashauri za wilaya ya Mpimbwe na Mlele zilipokea kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya elimu.
Aidha serikali ilitoa fedha kwa halmashauri hizo mbili kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 4.3 kwa ajili kutekeleza miradi ya maenedeleo ya Afya, kiasi cha zaidi shilingi Bilioni 3.1 ilielekezwa kutekeleza miradi ya Maji wilayani hapo.
Mhe. Sanga amefafanua kuwa kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 halmashauri hizo zimepokea pia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 937,977,000.00 ikiwa ni kwa ajili ya kutoa huduma ya umeme kwa jamii, pia kiasi cha zaidi ya Bilioni 5.2 kwa ajili ya miundombinu ya barabara.
MWISHO.
*Imetolewa na:*
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini.
*Halmashuri ya Wilaya ya Mpimbwe.*
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa