Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, leo tarehe 4 Aprili 2025, imepokea timu ya wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Ardhi kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya ardhi. Mafunzo hayo yametolewa kwa wajumbe wa vijiji, vitongoji pamoja na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mpimbwe, ikiwemo kijiji cha Chamalendi, kijiji cha Kashishi, Minyoso, Mirumba, Ikuba, Nyambwe, Mkwajuni, Msadya na mengineyo. Lengo kuu ni kuwafikishia wananchi elimu itakayosaidia kutatua migogoro ya ardhi, pamoja na kuwawezesha kupata hati miliki za maeneo yao kisheria. Wataalamu hao wameambatana na Mkuu wa Kanda wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Ndugu Emmanuel Magembe, ambaye ameongoza mafunzo hayo kwa kuzingatia umuhimu wa elimu hii katika usimamizi bora wa ardhi na kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo haya.
Katika mafunzo hayo, wataalamu wameeleza kwa kina malengo ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuwezesha usimamizi mzuri wa ardhi, kuhamasisha uzalishaji wenye tija, na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za ardhi kwa haki na usawa. Elimu hiyo imetoa msisitizo kwa wananchi kutumia ardhi kwa kuzingatia mipango iliyowekwa ili kuongeza thamani ya ardhi na kuchochea maendeleo katika jamii.
Aidha, wataalamu hao wameeleza kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi una faida nyingi kwa jamii, ikiwemo kuondoa migogoro ya ardhi baina ya watumiaji, kusaidia utunzaji wa vyanzo vya maji, kuzuia ufyekaji wa misitu na mapori yaliyohifadhiwa kwa matumizi maalum, pamoja na kuwezesha matumizi endelevu ya ardhi. Wananchi wamehamasishwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa