Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe imeungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kushiriki zoezi la upandaji miti lililofanyika leo tarehe 27 Januari 2026 katika Kituo cha Afya cha Usevya, Kata ya Usevya. Katika maadhimisho hayo, Rais Samia ametimiza umri wa miaka 66, huku tukio hilo likiwa na lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuendeleza uhai wa taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Shamimu Daudi Mwariko, alimpongeza Rais Samia kwa siku yake ya kuzaliwa na kumtakia afya njema, baraka na maisha marefu. Amesema miti ni uhai na nguzo muhimu katika utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa kupanda miti ni ishara ya uhai na ustawi wa Taifa la Tanzania. Ameongeza kuwa upandaji wa miti katika eneo la Kituo cha Afya cha Usevya unaonesha namna ambavyo Rais Samia amewekeza kwa vitendo katika sekta ya afya, ikiwemo utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaotarajiwa kuwa mkombozi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Ndugu Mwamle Saka, amesema halmashauri inaungana na Rais Samia katika dhamira yake ya kutunza na kuhifadhi mazingira. Ameeleza kuwa katika hafla hiyo jumla ya miche ya miti 400 imepandwa katika eneo la Kituo cha Afya cha Usevya, na kuongeza kuwa zoezi la upandaji miti litaendelea kufanyika katika kata zote tisa za Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupanda na kutunza miti.
Naye Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Usevya, Ndugu Geofrey Chundu, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupanda miti kwenye maeneo yao, akibainisha kuwa miti inalinda na kuboresha mazingira pamoja na kuchangia maendeleo endelevu. Ameongeza kuwa kushiriki zoezi hilo ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada zake za utunzaji wa mazingira, huku akimpongeza kwa siku yake adhimu ya kuzaliwa na kumtakia maisha marefu yenye afya njema.
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa