Saturday 21st, December 2024
@
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuanzia Juni mosi mwaka huu, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake yatakoma ifikapo Mei 31, 2019. “Hivi karibuni nimemwagiza Waziri anayesimamia masuala ya mazingira ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali, ikiwemo wenye viwanda vya kutengeneza mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuhakikisha jambo hili linatekelezwa kwa haraka.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumanne, Aprili 9, 2019 Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020. “Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia, wauzaji kuondoa mzigo uliopo, Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki,” amesema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua kwamba kuna baadhi ya bidhaa lazima zifungwe kwenye vifungashio vya plastiki na kwamba vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku. “Kwa msingi huo, katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yatatolewa maelezo ya kina kuhusu katazo la vifungashio vya aina hii, hasa katika maeneo ya uzalishaji viwanda, sekta ya afya, na kilimo,” amesema.
Waziri mkuu ana imani kuwa utaratibu huo pamoja na kutunza mazingira, utatoa fursa ya kutengeneza ajira nyingi husasan za watu wa chini kupitia utengenezaji wa mifuko mbadala ya plastiki pamoja na kutumia kikamilifu fursa ya viwanda vya karatasi vilivyopo nchini ikiwemo cha Mgololo. Amesema matumizi ya plastiki nchini yameendelea kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka.
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa