Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi imetekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kasim Majaliwa la Kituo cha Afya Majimoto kuanza kutoa huduma kwa Wananchi ifikapo 27 Desemba 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Hoza Mrindoko, 29 Desemba, 2022 ametembelea kituo hicho na kushuhudia huduma mbalimbali za Afya zikitolewa na Wataalamu wa Afya Kituoni hapo.
Akizungumza na Wananchi waliofika kupata huduma kituoni hapo Mhe.Mwanamvua ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe kwa kutekeleza kwa wakati Maagizo ya Waziri Mkuu ambapo amewataka Wananchi wa Majimoto kuendelea kutunza miundombinu ya Kituo hicho cha kutolea huduma za Afya.
Mhe.Mrindoko amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Wilayani Mlele kuharakisha Ujenzi wa Nyumba za Watumishi kituoni hapo ili waweze kuwa karibu na Mazingira ya kazi ili Wananchi waweze kupatiwa huduma kwa wakati.
Aidha Mhe.Mrindoko amesisitiza Wananchi wa Majimoto kutoa ushirikiano kwa Viongozi ikiwa ni pamoja na kutoa Taarifa kwa vyombo husika iwapo watabaini upotevu wa Dawa na Vifaa tiba.
Mnamo Tarehe 14 Desemba, 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa alifanya ziara Wilayani Mlele katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe ambapo alitembelea Kituo cha Afya Majimoto na kutoa maagizo ya kituo hicho kuanza kutoa huduma kwa Wananchi ifikapo 27 Desemba 2022.
Mwisho.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Mawasilino Serikalini .
Halmashauri ya Mpimbwe.
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa