Na. Odetha Salumu
Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filbarto Sanga amefanikiwa kurejesha hekari sabini (70) kwa wakulima zilizokuwa zimemilikiwa kinyume cha sheria na mkulima aliyejulikana kwa majina ya Chenge Samsoni mkazi wa kijiji cha Ikulwe Kata ya Majimoto wilaya ya Mpimbwe mkoa wa Katavi.
Akizungumza na wananchi katika ukumbi wa shule ya msingi Majimoto, Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Filbarto Sanga akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe Bi. Catherine Mashalla, Mkuu wa Idara ya Ardhi Evaline Meray, Diwani wa kata ya Majimoto Mhe. Grace Udoba pamoja na watendaji ngazi ya Kijiji na kata hiyo amekemea tabia ya wananchi hao kujimilikisha maeneo ya serikali ya kijiji kinyume na sheria.
"Ninatoa rai kwa wananchi wangu wa eneo hilo, ni kosa kubwa kujimilikisha eneo ambalo si mali yako halali kwani kufanya hivyo kutachangia kuibuka kwa migogoro mingi ya Ardhi katika maeneo haya"
Awali, kipokea maelezo kutoka kwa wananchi wa eneo hilo, imefahamika kuwa jumla ya hekali 169 zilitengwa kwa ajiri ya malisho ya mifugo, baadae walijitomeza wananchi watano akiwemo Chenge Samsoni, Richard Mashelia, Obeid Bunzali, Emmanuel Kipozi na Bundala Lukuba wote wakiwa ni wakulima katika Kijiji hicho kutaka kuligawana eneo hilo kinyume na sheria hali ambayo haikufanikiwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya wananchi hao wamefafanua mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa Serikali ya kijiji cha Ikulwe ilichukua jukumu la kuligwa eneo hilo kwa wananchi ambapo kila mwananchi aliuziwa hekari 1 kwa shilingi elfu hamsini (50,000.00) na kiasi cha shilingi elfu tano (5,000.00) ililipwa na mwananchi alienunua eneo hilo kwa ajili ya upimaji.
Malalamiko hayo yamekuja kufuatia mkulima aliejulikana kwa jina la Chenge Samson mkazi wa eneo hilo kulima jumla ya hekari sabini (70) Mali ya wakazi wa Kijiji na kata ya Majimoto.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Bi. Catherine Mashalla alipokea Malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo hilo hali ambayo ilipelekea October 19, 2022 kufanya kikao cha utatuzi wa mgogoro huo, lakini mlalamikiwa Chenge Samson aliondoka kabla ya kikao kuanza hivyo ikamlazimu Mkurugenzi Bi Mashalla kuwataka wakulima kuendelea na shughuli za kilimo katika maeneo yao halali.
"Kwa kuwa nimemuita huyu bwana Chenge Samson na akaamua kupuuzia wito huu kikaoni nawaomba wananchi mkaendelee na shughuli za kilimo katika maeneo mliyouziwa awali pasipo kusumbuliwa na mtu yeyote" Alisema Mkurugenzi Bi. Catherine Mashalla
"Mkuu wetu wa wilaya Mhe Sanga atakuja kesho kutoa ufafanuzi ili haki yenu ipatikane" Alisema Mkurugenzi Bi. Catherine Mashalla
Mara baada ya Mkuu wa Wilaya kusikiliza maelezo ya wananchi na kurejea maamuzi ya mkurugenzi, Mhe. Sanga akiwa kikaoni hapo amewataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu wakati wanapotaka kuuza ardhi yao na waepuke kuuza Ardhi holela pale mtu anapokuwa na shida.
"Ninawasihi wananchi wangu, tuepuke kuuza Ardhi yetu kiholela kila unapopata shida nyumbani kwako, ardhi ni mtaji, ardhi ni maisha na ardhi ni muhimu kwa maisha na maendeleo ya familia zenu, tuitunze na tuepuke kutengeneza migogoro ndani ya eneo hili"
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Mleme Mhe Sanga amewaagiza wakulima hao kuendelea kulima mashamba yao na endapo watazuiliwa na mtu huyo alieamua kujichukulia maeneo hayo na kuyalima kinyume cha sheria watoe taarifa kwa uongozi wa wilaya haraka ili hatua za kisheria ziweze kufuatwa.
"Wananchi, ninawaomba mkaendelee na shughuli zenu za kilimo katika maeneo yenu aliyoyalima huyo bwana Chenge Samson, asiwatishe, katika vikao vyote cha mkurugenzi na changu hayupo ni mtu wa aina gani huyu, tutachukua hatua za kinidhamu kwa yeyote atakae jaribu kuwaonea wananchi" amesema Mkuu wa Wilaya Mhe. Sanga
Ikumbukwe kuwa Mlele ni wilaya mpya katika mkoa mpya wa Katavi, ambavyo vyote vilianzishwa rasmi mnamo Machi 2012, maeneo yake yalikuwa sehemu ya wilaya ya Mpanda na makao makuu ya wilaya yako Inyonga.
Katika zoezi la sensa ya watu na makazi la mwaka 2012 idadi ya wakazi ilikuwa watu katika Wilaya hiyo ilikuwa ni watu laki mbili themanini na mbili elfu mia tano sitini na nane (282,568), wilaya ya mlele Ina jumla ya kata ishirini na nne ikiwemo kata za Ikuba, Ilela, Ilunde, Inyonga, Itenka, Kapalala, Kasansa, Kasokola, Kibaoni, Litapunga, Machimboni, Magamba, Majimoto, Mamba, Mbede, Mtapenda, Mwamapuli, Nsenkwa, Nsimbo, Sitalike, Ugala, Urwila, Usevya na Utende.
*Mwisho*
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano.
Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa