Serikali Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi imesimamamia utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu likitaka kufanyika makabidhiano kati ya uongozi wa zamani na uongozi mpya wa Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Mpimbwe (WMA).
Kabla ya kutembelea mipaka ya Jumuiya ya hifadhi ya wanamapori ya Mpimbwe, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga akatoa wito kwa viongozi wapya kutoingiza siasa katika uhifadhi badala yake watangulize uzalendo.
Kisha, Mkuu wa wilaya aliyeambatana na kamati ya ulinzi na usalama akaongoza msafara kukagua mipaka ya WMA Mpimbwe, hiyo ikiwa ni oparesheni maalmu ya kupitia mipaka ya maeneo ya Umma na misitu iliyohifadhiwa.
Msafara ukiwa katika pori hilo, umekuta maeneo mengi yamevamiwa na shughuli za kibinadamu zikiendelea jambo lililomfanya mkuu wa wilaya kutoa maagizo kwa uongozi wa Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Mpimbwe kufanya doria ili kuwabaini wavamizi na kuwaondoa.
Kwa upande wao mwenyekiti mpya wa jumuia hiyo, Domician Msakaile pamoja na Afisa Uhifadhi daraja la pili, Mollel ambaye msaidizi wa kitengo cha ulinzi hifadhi ya Taifa ya Katavi wameahidi kushirikiana ili kulinda maeneo hayo na hifadhi kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mpimbwe, Shamim Mwariko amesema halmashauri itaendelea kuwalea na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu ili kuhakikisha jamii haiharibu eneo hilo la WMA
Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Mpimbwe lilianzishwa na vijiji wanachama vitano mwaka 2006 na linaukubwa wa KM za mraba 667.95.
Pori hili ambalo lipo kwenye bonde la ufa, lina aina mbalimbali za wanyama kama vile tembo, samba,chui, duma, nyati, Twiga , Pundamilia na wengine.
Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe- Usevya
Sanduku la Posta: 245
Telephone: 0625732265
Mobile: 0625732265
Barua Pepe: ded@mpimbwedc.go.tz
Haki miliki @2017 Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe. Haki zote zimehifadhiwa